Tuesday, 30 August 2016


NIREHEMU
sehemu ya kwanza.

Ninavurugwa akilini, nateseka mtimani,
Yafanywayo duniani, yanikeketa maini,
Nimebaki 'le kaini, kuzurura duniani,
Kujuana ndiyo lugha, Maulana nirehemu.

Nilizawa kijijini, peke yangu nikasoma,
Kafanikiwa somoni, bila walimu kugoma,
Kazindikishwa chuoni,  nazo nyimbo za wamama,
Kujuana ndiyo lugha, Maulana nirehemu.

Lipofika  na chuoni, kawa yule duduvule,
Kakesha maktabani, Nikiwazia kilele,
Kajinyima na  rahani, nikaishi kama kale,
Kujuana ndiyo lugha, Maulana nirehemu.

Yangu minne kaisha, Nikashukuru Kahari,
Safari ya kunichosha, kaita mwisho dahari,
Hakuna takayetisha, na shahada mi hatari,
Kujuana ndiyo lugha, Maulana nirehemu.

Viwandani kwa madaha, ninabisha bila hofu,
Katibu kwayo furaha, karibu keti, halafu,
Vyeti  mi kwa ufasaha, navishika kimkufu,
Kujuana ndiyo lugha, Maulana nirehemu.

umealikwa na nani, ninaulizwalizwa,
Hajui mimi mghani, akilini naduwazwa,
Tabasamu ya usoni, wa katibu yalemazwa,
Kujuana ndiyo lugha, Maulana nirehemu.

Acha stakabadhizo, bi mrembo 'naropokwa,
Kwake  mekuwa chukizo, na maswali yakachokwa,
Mdomoni nina 'wozo, kwenye koo nimefikwa,
Kujuana ndiyo lugha, Maulana nirehemu.

Wiki mbili zakatika, simu yangu kitazama,
Nasubiri 'le dakika, taitiwa na yule mama,
Kijijini kusifika, huku ndo sasa kusoma?
Kujuana ndiyo lugha, Maulana nirehemu.

Sasa kesho nimepanga, kurudi  na viwandani,
 Za Nauli nimetenga, lipata kibaruani,
Safari nitaifunga, nikatange mjini,
Kujuana ndiyo lugha, Maulana nirehemu.

mikosi ya mla mbivu/ mjomba Paulo.